Pages

Friday, September 18, 2015

MGOMBEA KAWE ATEMBELEA MABWEPANDE NA BUNJU




Mgombea wa Ubunge jimbo la Kawe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kippi Warioba ametembelea kata za Bunju na Mabwepande ili kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi hao.
Akiwa katika kata ya Bunju, Warioba alikagua mradi wa daraja la Burumawe ambapo wananchi walitoa kero zao juu ya ucheleweshwaji wa ujenzi wake jambo linaloathiri shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

Wakazi wanaotumia daraja hilo walisema walijaribu kufuatilia jambo hilo kwa Diwani, Mbunge na Mkuu wa wilaya lakini hawaoni maendeleo yeyote juu ya utekelezaji wake nakuwafanya kuwa na hofu juu ya mvua za El Nino zinazotarajiwa kuanza kunyesha nchini hivi karibuni.
“Tumefuatilia kuanzia kwa  mwenyekiti wa serikali za mtaa na taarifa zilienda mpaka kwa rais wakati mvua ziliponyesha na kusababisha maafa,”alisema Noel Luchwani aliyewahi kuwa mwenyekiti wa mtaa wa Boko/Dovya.
Mkazi wa Boko Kati, Rose Komba alisema kucheleweshwa kwa ujenzi wa daraja la Burumawe unawarudisha nyuma huku wakinamama wakishindwa kupata huduma za afya kwa wakati.
“Wakinamama wengi wanajifungulia njiani kwa sababu hakuna njia inayopitisha gari kuwafikia walipo, watoto wetu wanashindwa kwenda mashuleni hasa kipindi cha mvua. Shughuli za wajasiriamali pia zimesimama kwa maana hakuna njia ya kupitisha bidhaa barabara tunayoitegemea ni hii jambo linarudisha nyuma uchumi wetu.”
Akiwa katika Kata ya Mabwepande, Warioba alitembelea eneo la Mji Mpya ambalo lilikua maalumu kwa wahanga wa mvua kubwa zilizonyesha jijini hapa mwishoni mwa mwaka 2011. Wakazi hao walilalamika kukosa huduma muhimu kama maji, soko, upungufu wa matabibu, maeneo ya kuzikia, kufanyia ibada na viwanja vya michezo.
“Hatuna eneo maalumu la kuzikia wapendwa wetu wala soko kwa sababu lililopo liko mbali sana hivyo tunalazimika kutumia pikipiki ambayo ni gharama ukizingatia sisi bado kipato chetu hakiko imara tangu tuhamie huku”, alisema Mwantumu Nawaz, mkazi wa Mji Mpya.
Diwani wa kata ya Mabwepande (CCM) anayemaliza muda wake, Clement Boko alisema maeneo yalishatengwa na taarifa zipo kwenye ofisi ya Ofisa Mipango Miji.
“Vitu viko kwenye utekelezaji na taarifa nimeshapeleka kwa Ofisa Mipango Miji ili tupate maeneo ya soko, kuabudia na kuzikia. Tunasubiri wao tu kuja kutuonyesha ni wapi wameandaa kwa ajili ya shughuli hizo”, alisema Boko.
Warioba aliahidi kufuatilia kwa sehemu husika ili kuhakikisha kero hizo zinatatuliwa hasa ukizingatia kuna mvua za El Ninyo zinazotarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa.
 


No comments:

Post a Comment